Na Rev. Canon Francis Omondi

 

Serikali yetu inaamua kunyonya biashara maskini na kujaribu kuita ni fadhila.

Kuweka Kodi ya Mauzo (TOT) ya 3% kwa biashara ndogo zisizo rasmi ni ukatili, na ni dharau kwa wakenya dhaifu. Ingawaipo kisheria, lakini TOT ni batili. Natamka tamko la kinabii: “Ole wao wanaotunga sheria zisizo za haki, watu wanaopitisha sheria za kukandamiza, Huwanyima maskini haki zao, na kuwaibia maskini wa watu wangu maslahi yao…” (Isaya 10:1)

Biashara ndogondogo, vioski, maduka rejareja, saluni au wachuuzi wadogowadogo, tabaka la chini kabisa la sekta isiyo rasmi, sasa wanatakiwa kulipa TOT. Kodi inayotozwa kwa mkazi yeyote ambaye mauzo yake hayazidi au hayatarajii kuzidi Ksh. 5,000,000 kwa mwaka wowote wa mapato. Italipwa kuanzia 1 Januari 2020. Wanatoza kiwango hiki cha ushuru kwenye mauzo ya jumla / faida na ni ushuru wa mwisho. Bi Elizabeth Meyo, Kamishna wa Ushuru wa ndani katika Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA), anasema kwamba “kuanzia Januari 2020, ikiwa mtu atafanya kazi saluni, buchani, au duka la rejareja, atahitajika kutangaza mauzo yake mtandaoni na kulipa ushuru tarehe 20 ya kila mwezi. “Na kwa mtu kupata leseni ya biashara kutoka serikali ya kaunti yake, atalazimika kulipa nyongeza ya asilimia 15 ya kibali cha KRA kama ushuru wa awali. Kutokana na vigezo hivi vipya, Bi Meyo anaongeza kusema, “wamiliki wa biashara watakuwa wametimiza wajibu wao wa kizalendo kwa Kenya bora”.

Tafiti kadhaa za uchumi zinasifia mchango mkubwa wa sekta isiyo rasmi katika nchi nyingi zinazoendelea katika mapato ya nchi zao. Sekta isiyo rasmi ni moja ya waajiri wakubwa nchini Kenya, na inatoa zaidi ya asilimia 80 ya fursa za ajira. Ni aibu kwamba macho ya watawala yamegeukia kwenye sekta hii tu kwa sababu ya pesa zao, na kuziba pengo linalotokana na kupungua kwa mapato kutoka kwa sekta rasmi. Kulingana na Zachary Mwangi, matumizi ya kila mwezi  ya mishahara na ujira kwa Biashara ndogondogo na za Kati (MSEMs) ilikuwa Ksh bilioni 9.0 ambayo ni sawa na asilimia 25.0 ya jumla ya mapato. Idadi ya watu wanaojihusisha na biashara ndogondogo na za kati (MSEM) ilikuwa takriban milioni 14.9 na biashara ambazo hazisajiliwa zinachangia 57.8%. Wafanyikazi wanaolipwa walikuwa milioni 4.0.

Mfumo wa masoko wa kikoloni bado unaendelea kutawala uchumi wetu, ambao unatufanya tuione sekta isiyo rasmi kuwa duni kuliko ile iliyo rasmi. Bado tunaiona ‘ya chini’, pembezoni au pembeni na isiyo na uhusiano wowote na uchumi rasmi wa maendeleo ya kisasa ya viwanda. Kwa hivyo tumepuuza sekta hii. Wachumi wengine wameielezea kamadimbwi la ajira lenye wafanyakazi waliokosa sifa za kuingia katika sekta rasmi. Wengine kama Jeffery Sachs wamekwenda mbali zaidi na kutamka kuwa sekta isiyo rasmi itapotea kabisa Kenya itakapofikia viwango vya juu vya ukuaji wa uchumi na viwanda.

Wengine waliona nguvu ya biashara ndogondogo za sekta isiyo rasmi. Mchumi De Soto (1989) aliona biashara hizi zisizo rasmi kama ishara ya ari ya ujasiriamali, na nguvu halisi katika soko. Na inaweza kunyanyua viwanda, kwa sababu ya ustahimilivu wao na uwezo wa kuhimili mitikisiko ya masoko kwa muda mrefu kama Shem Watako alivyoona katika masomo yake ya udhamivu ya biashara ndogo ndogo huko Kariobangi. (2016: 204)

Ujasiri huu wa sekta isiyo rasmi ndio umewavutia watoza kodi. Lakini changamoto ni jinsi watakavyotekeleza hii TOT. Bi Meyo anaainisha ugumu huu, wakati akijibu ni kwanini Kenya iliamua kuweka TOT kwenye biashara ndogondogo, “kukosekana kwa muundo rasmi na mfumo wa ushuru unaolingana na sekta hiyo kumekuwa kikwazo kikubwa kwa tamaa ya ‘watoza ushuru’ kuchota mapato kutoka kwa sekta hii.”

Hoja ya kimaadili ya wale wanaowaita wafanyabiashara wadogowadogo kulipa ushuru kama inavyodaiwa, haiwezekani, kwa sababu haijibu swali la pili. Je! Ni sawa kuweka hivi kwa biashara masikini zaidi za Kenya?

Je ni maadili kuwapuuza masikini , wakati mfumo mpya wa kodi utawanyonya?

Hebu tuangalie mfano wa biashara inayoendeshwa na Achieng ‘, ” Nyamulu Beauty Salon”, huko Kariobangi ili kuonyesha ukweli huu. Pamoja na mapato yake ya Ksh. 100,000 kwa Januari 2020, bado TOT inamhusu.

Kodi ya mauzo (TOT) ni kama kodi ya ongezeko la thamani (VAT), tofauti yake ni kwamba inatoswa papo hapo kwa bidhaa za mtaji, kama Kimaru na Jagongo wanavyosema. Ni kwa msingi wa ‘ad adorem’ (kulingana na thamani ya bidhaa husika, badala ya kuwa kiwango sawa), inayotumika katika mchakato au ngazi ya uzalishaji. TOT inafanya maskini kulipa kodi nyingine isiyo ya moja kwa moja, wakati wale wenye mtaji wa zaidi ya milioni 5 watalipa kodi ya moja kwa moja ambayo ni mpango bora wa ushuru kwa biashara zao.

MFANO WA NYAMULU BEAUTY SALON, YA KARIOBANGI.

 

KIPENGERE MAPATO/GHARAMA USHURU & KODI  
Mapato kwa wateja 100 @ 1000                  100,000    
Gharama pungufu      
Umeme                    (5,000) VAT +Kodi                (901)
Malighafi (Mafuta, nywele, n.k.)                  (30,000)  VAT @16%             (4,800)
Kodi ya chumba                  (12,000)  Kodi ya kodi ya pango@10% Incl             (1,091)
Wafanyakazi 2@500 a day                  (30,000)    
Ushuru wa Mshwari                    (5,850)    
Leseni ya kaunti                    (1,250)  Leseni ya kaunti             (1,250)
Faida ya uendeshaji wa biashara                    15,900  Jumla ya kodi & ushuru             (8,042)

Matarajio

VAT huoangwa kwa kila bidhaa na huduma

MFANO WA 1 -TOT
Faida ya Uendeshaji Biashara                    15,900    
Kodi ya mauzo pungufu                    (3,000)  Jumla ya kodi & Ushuru
Faida halisi                    12,900   11.04%

 

MFANO WA 2- Kodi ya mapato binafsi
Faida ya biashara                    15,900    
PIT –Baada ya msaada                        (362)  Jumla ya kodi  & Ushuru             (8,404)
Net Profit                    15,538 Asilimia ya kodi 8.4%

 

MFANO WA 3 Kodi ya mapato binafsi na VAT ikihusishwa
Faida ya uendeshaji wa biashara                    15,900    
VAT ya mtaji ikiondolewa      
Umeme                          664    
Malighafi                       4,800    
Faida halisi/mapato ya kutozwa kodi                    21,364    
PIT -Baada ya msaada                    (1,182)  Jumla ya kodi & Ushuru             (3,760)
Faida halisi                    20,182 Asilimia ya kodi 3.76%

Mfano wa 3 unatia moyo wafanyabiashara wadogo kujisajili kwa VAT ambayo inakwenda hadi kwa wateja; athari ni kuongezeka kwa uwazi na kuongezeka kwa makusanyo ya VAT kwa KRA.

 

 

TOT  PIT PIT +VAT Reg
Faida                  12,900                   15,538               20,182
Kodi                  11,042                      8,404                  3,760
Asilimia ya kodi % 11.04% 8.4% 3.76%

 

 

Mpango mbadala wa ushuru badala ya TOT ungekuwa na matokeo tofauti. Ikiwa mifano ya apo juu imeelezea biashara yake, basi kwa mfano wa kwanza ambapo angelipa TOT, faida yake ingekuwa Kshs. 12,900. Katika mfano wa pili ambapo analipa kodi ya mapato binafsi, faida yake ingekuwa Ksh. 15,538. Na kama angesajiliwa VAT na analipa pia PIT, angefanya faida ya Ksh. 20,182.

Kwa hiyo mpango wa ushuru wa mmoja mmoja ungefaa zaidi kwa makundi ya biashara ya kipato cha chini kuliko TOT.Utaona pia kuwa biashara yake imechangia kwa namna nyingine mapato ya serikali ya Ksh. 8, 042. Halafu kamaikihusisha TOT ya Ksh. 3000, angechangia Kshs. 11,042 kwa mapato ya serikali.

 

Je ni sawa kwamba mamlaka ya kodi inamong’onyoa mtaji wa masikini?

Mtaji wa kianzio kwa biashara ndogo ndogo hutokana na rasilimali za familia, kulingana na McCormick et al. (1997) hii huathiri ukubwa wa biashara zao, idadi ya wafanyakazi ambao wanaajiri, na kiwango cha faida wanayopata. Kwa hivyo, wanakuwa na kiasi kidogo kinachopatikana kuwekeza tena. Mwangi (KNBS 2016) anasema kuwa biashara ndogo ndogo zilizosajiliwa ziliripoti kutumia asilimia 45.3 ya mapato yao yote kwa uwekezaji, iwe kama kujazia mtaji au kuwekeza katika biashara mpya na uwekezaji katika kilimo, wakati matumizi kwa ajili ya kaya na familia yanahitaji asilimia 44.5. Mnamo mwaka wa 2016, Mwangi anabainisha, biashara ndogo na za kati zilitumia kwa kiasi kikubwa sehemu ya mapato yao kwenye uwekezaji kwa asilimia 63.4 na 69.7.

Mmomonyoko wa mtaji kwa biashara ndogo kwa njia hii, kutachelewesha sana jitihada zao za kuutoroka umasikini. Badala yake, kuwaruhusu kukuza mtaji kungesaidia kukanusha mtazamo unaoshikiliwa na wengi ikiwa ni pamoja na ILO (2002) inayounganisha sekta ndogo ya biashara na umasikini, kwa sababu wanapata kidogo kwa wastani kuliko wale walio kwenye kazi rasmi. Kwa maana, kama Watako (2016) alivyogundua, “idadi kubwa ya wajasiriamali kwenye sekta isiyo rasmi wanapata zaidi, kwa wastani, kuliko wafanyikazi wasio na ujuzi katika sekta rasmi”.

Sio uungwana kuwanyima masikini nafasi ya ushindani sawa katika soko kwa kuwaongezea kodi kwenye biashara zao.

Serikali zimetumia ushuru kunyamazisha sehemu ya uchumi. Cheeseman, N., & Griffiths, R. (2005) anasema kwamba ushuru wa mauzo unaweza pia kuwa adhabu kama umeundwa kukwamisha kununua bidhaa fulani. Wanasema sheria za mazingira wakati mwingine huhimiza suala hili, kuwanatoza watu zaidi juu ya ununuzi wa vitu vinavyoharibu mazingira.

Licha ya asili ya ugumu kwa sekta hii, mamlaka kuwalenga Tabata la chini ambalo linahenya na mzigo wa madeni ni kukosa ubunifu na ni uovu. Tunaona TOT kama jaribio la kuyakata kabisa kutoka kwenye soko. Hizi biashara ndogo ndogo nchini Kenya, kulingana na uchunguzi wa serikali wa 2010, ziliajiri watu wapatao milioni 2.4, sawa na 17% ya wafanyikazi nchini Kenya mnamo 2009. Wanajihusisha kama ifuatavyo: karibu na 2 /3 Theluthi mbili – 64.1% ya biashara zote zilikuwa kwenye sekta ya uchuuzi. Biashara za rejareja zilichangia 62% ya biashara zote nchini Kenya. Viwanda hufanya 13% wakati huduma 15% (Watako 2016: 207).

Sio uungwana kwa serikali kuwatwisha mizigo bali kugawanya maslahi kwa usawa kwa masikini.

Katika demokrasia huria, anasema Prof Nicholas Wolterstorff wa Shule ya Biblia ya Yale, serikali haipaswi kuwa na  upendeleo wakati wa kugawa wajibu na maslahi kwa raia wake. Serikali yetu haipo katika maisha ya raia hawa masikini, kwa sababu ya vipaumbele vya maendeleo vilivyowekwa. Wanaishi katika makazi duni, na watoto wao wanaohudhuria shule zilizosongamana, wanakosa huduma za afya, watumiaji wakuu wa usafirishaji wa umma wowote unaobakibarabarani na wanaohitaji chakula cha kutosha. Lakini sasa wanafurahia kuwatoza ushuru wafanyabiashara hawa wa tabaka la chini kabisa la taifa letu, wakiwa ama katika makazi duni ya mjiji na miji yetu au maeneo ya vijijini. Kupitia biashara zao wameboresha mengi sana. Watako (2016: 209) anaonyesha jinsi wajasiriamali wadogo wadogo huko Kariobangi alivyochochea ustawi wa maeneo, hasa mahitaji ya msingi: shughuli za biashara; upatikanaji wa huduma ya afya; upatikanaji wa elimu; upatikanaji wa makazi; upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira; njia bora za usafirishaji; kuongezeka kwa chakula na mapato.

Tunaweza kutumia ushuru kwa uzuri, hata kwa kuondoa uonevu katika jamii na kutoa huduma sawa kwa raia wote. Eric Nelson profesa wa Harvard, anafafanua wazo hili kwamba serikali inapaswa kudhibiti kikamilifu ugawanywaji wa mali kwa sababu ni jukumu la serikali kujihusisha na ugawaji wa mali kupitia ushuru hivyo kuhakikisha ustawi wa watu masikini, na huo ndo mwanzo wa ustawi katika nchi nyingi za Ulaya.

Kulazimisha ushuru bila kujali hali ya biashara ya walipaji inakumbusha kicha ya pango na kichwa ya Kikoloni ya 1920s. Halafu, viongozi wenyeji na mwakilishi walitetea watu wao dhidi ya unyonyaji wa wakoloni. Katika kujibu mahitaji ya koda, viongozi wa Luo huko Nyanza walishauriana na wakaita mkutano mkuu huko Lundha, Gem mnamo tarehe 23 Desemba 1921. Karibu watu 9000 walihudhuria kutoka sehemu zote za Nyanza kujadili shida hiyo kwa mara ya kwanza. Wakajadili kodi ya Pango. Wakati wa mkutano Mkuu Ogada Odera wa Gem huko Nyanza ya kati alilia: “Kuhusu kodi zetu, zilikuwa sh. 3. Bwana John Ainsworth (Kamishna wa Mkoa wa Nyanza kule Kisumu kutoka 1906) alituambia kwamba kiasi hicho kitaongezeka hadi sh. 5, tulikubali. Serikali sasa imeongezeka hadi sh. 8. Ni nzito sana. Mbali na hilo, hatutaki wanawake wetu walipe ushuru. ”

Chifu Ogada, alitoa maoni yake: “Kuhusu neno koloni, serikali ilikuja hapa na kutukuta tukiwa na kazi na sasa inatuita ‘wasumbni’ (watumwa wao)”. Alikuwa akielezea kuwapa watu wake ufahamu kuhusu mabadiliko.

Watoa maoni wengi juu ya TOT wameunga mkono msimamo wa serikali na unyonyaji wa biashara duni kwa kuiita ni haki, uzalendo, rahisi kutekeleza na kukamilisha. Nadhani wako nje ya uhalisia.

Kuna mtazamo wa jumla wa mapato makubwa katika sekta isiyo rasmi. “Lakini serikali haikuwa ikipata faida yoyote ya kodi kutoka kwa biashara hizi,” Kamotho Waiganjo anaandika, “… wale wanaofanya kazi katika tasnia rasmi, na walio kwenye uangalizi wa mamlaka ya kodi, … wanalipa hadi asilimia 30 ya faida ya kila mwaka kama kodi, … biashara katika sekta isiyo rasmi inamaanisha kwamba wafanyabiashara wengi katika tasnia hii ghali hukwepa mitego ya mamlaka ya kodi. Haitakuwa hivyo tena.”

Fikra hii, kwamba masikini katika sekta hii huchuma kiasi kikubwa cha mapato lakini hawachangii kwenye kapu la ushuru, ni makosa. TOT ni ushuru usio wa moja kwa moja wa biashara na sio ushuru unaotokana na mapato ya faida ya biashara. Biashara za sekta isiyo rasmi tayari hulipa kodi zingine zisizo za moja kwa moja, kwenye mafuta, umeme, VAT kwenye bidhaa zao na kodi ya pango inayokusanywa kutoka kwa kodi zao. Ikiwa watalazimika kulipa kodi ya nyongeza, je! Sivyo pia wanapaswa kulipa kodi kutoka kwa mapato yao nje ya biashara, ambayo huja chini ya ushuru wa mapato binafsi na sio 30% ambayo makampuni wanalipa? Je! Si kwamba gharama za bidhaa, gharama za biashara, na misaada yao mingine pia itahusika?

Wengine wanasema kuwa gharama ya kukidhi vigezo ni ndogo. Inahitaji nyaraka chache za walipa kodi katika eneo hili.Kinachohitajika ni rekodi ya mauzo yao tu. Wale wanaolipa ushuru wa mauzo hawatahitaji kuwa na wasiwasi juu ya kufuatilia matumizi yao, ushuru wao uko kwenye mauzo. Inamaanisha kwamba nyaraka muhimu mkubwa kwa wafanyabiashara ni kuonyesha mauzo yao tu.

Sasa hii ni kuweka kikwazo katika njia ya kipofu. Kuweka rekodi sahihi za biashara kuna faida nyingi kwa wamiliki wa biashara sio tu kwa TOT. Rekodi sahihi zinaweza kuwaongoza wamiliki wa biashara kutathmini utendaji wao wa biashara, kufuatilia gharama za ununuzi na mauzo, wadai na wadaiwa na kusaidia katika kufanya maamuzi muhimu ya biashara. Maskini anapaswa kushauriwa.

Matokeo ya unyonyaji biashara ndogondogo yatakuwa janga kwa sababu ya umuhimu wa sekta hii katika uchumi. Inaweza kuamsha miitikio mikubwa miwili kutoka kwa masikini:

Kwanza, ikiwa biashara ndogo ndogo zikinusa unyonyaji, zinaweza kutoweka kwa na kupotea. Biashara zinahisi kiurahisiunyonyaji wa mamlaka na zinaweza kutulia, kurekebisha shughuli zao hadi hali itapobadilika. Uharibifu baada ya kutoweka kwao unaweza kuwa mkubwa. Bwana Francis Atwoli Katibu Mkuu wa Jumuiya kuu ya Vyama vya Wafanyabiashara (COTU) kufuatia tathmini yake alionya kwamba kuweka ushuru zaidi kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati sio tu kutaharibu sekta inayokua kwa kasi ya uchumi lakini pia itawapa Wakenya wengi kukosa kazi.

Uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa ya Kenya (KNBS) ya 2016 unaonyesha kuwa takriban biashara 400,000 ndogondogo na za kati hazisherehekei siku yao ya pili ya kuzaliwa. Wachache hufikia siku yao ya kuzaliwa ya tano- inaonyesha wasiwasi wa uendelevu wa sekta hii muhimu. Wanaposhinikizwa, hutoweka hewani.

Pili, ikiwa wamiliki masikini wa biashara watatafsiri kodi hii kama ukandamizaji, wataasi. Utekelezaji wa TOT utaamshamaumivu ya enzi za ukoloni. Kodi ya pango na kichwa ilikuwa mzigo mzito kwa watu wa Kenya katika miaka ya 1920. B A Ogot (2009: 772) anaona kuwa ilifanya vibaya zaidi na njia ya ukusanyaji ambayo ilikuwa ya kikatili na ya hovyo. Huko Nyanza, walikusanya Ushuru wa pango kwa vibanda vyote huko Kraal, pamoja na ‘duol’ na ‘abila’ (Mazizi ya mifugo). Wakati watu wengi walikataa kulipa kodi hizi, wakuu wa wakoloni wakiwemo wakuu na makarani wa kodi walitumia njia za kikatili za ukusanyaji, wakawaamuru wakuu wa polisi na machifu kuvamia vijiji, kuchoma nyumba, kuchukua mali au vitu vya chakula kama vile nafaka, ndizi na mihogo.

Kwakuwa TOT itakula maisha ya wamiliki hawa wa biashara, wataasi. Lakini watakomesha uasi wao, kwa kukosa uwezo uongozi kama vikundi vya kupinga kodi ya kichwa kule Uingereza mwaka 1990. Kuanzisha “kodi ya kichwa” ni suala liliomlazimisha Bi Margaret Thatcher kuachia ofisi mnamo Novemba 1990.

Jarida la kijani la 1986, Kulipa Serikali za Mitaa, ilipendekeza kodi ya kichwa, ambayo ilitoza kiwango fulani cha kodi kwa kila mtu mzima kwa huduma zinazotolewa katika jamii yao, ndio maana ya neno ‘kodi ya kichwa’. Ilikuwa mabadiliko kutoka kwa malipo kulingana na thamani ya nyumba ya mtu hadi mkazi mmoja mmoja. Kodi hiyo, ilipingwa kuwa haikuwa sawa, na mzigo mzito kwa wale wasio na uwezo. Kilichofuata ni maandamano na ghasia zilizosababisha kukomesha kodi kufuatia mabadiliko ya serikali ya kihafidhina Novemba 1990.

Nini KRA ifanye kwa biashara masikini?

Serikali na KRA kama chombo kinachotekeleza wanaweza kutenda wema kwa kuzuia kuumiza biashara za watu masikini. Wanaweza kuifanya iwe sera ya kipaumbele kurekebisha sekta isiyo rasmi badala ya kuifuta kupitia sera kali za kodi. Kodiya mapato kama ilivyotungwa ni hiari, ambayo biashara ndogo zenye sifa zinaweza kuamua kujisajili kwa mfumo wa kawaida wa kodi. Hatua hii ingewaruhusu kutambuliwa kama biashara zingine. Rekodi makini, kuhusishwa sheria na mchakato wa kupunguza ambao unahitajika katika kuthibitisha matumizi. Tunapaswa kufanya bidii katika kusaidia biashara za watu masikini, kutunza rekodi sahihi za biashara na kuwawezesha kuingia katika mpango mbadala wa kodi.

Serikali hii inapaswa kutii maneno ya Hubert Humphrey, Makamu wa Rais wa zamani wa Marekani, wakati wa kuwekwa wakfu kwa Jengo la Hubert Humphrey mnamo Novemba 1, 1977, alisema: “Mtihani wa maadili ya serikali ni jinsi serikali hiyo inavyowatenda wale ambao wanaanza maisha, watoto; wale ambao wako katika mapambazuko ya maisha, wazee; wale ambao wako kwenye vivuli vya uzima, wagonjwa, wahitaji na wenye ulemavu. ”

The tinders are there waiting for something to ignite them. If the poor interprete these as days of extortion, we may as well have ushered in days of revolt.

Kuni ziko tayari zikisubiri kitu cha kuziwasha. Ikiwa maskini wanatafsiri kama hizi siku za unyonyaji, tunaweza kutumbukia sote kwenye siku za machafuko.

 

Canon Francis Omondi ni kuhani wa Dayosisi ya kanisa kuu la Watakatifu Wote, katika Kanisa La Anglikana La Kenya. Yeye pia ni mhadhiri wa msaidizi katika Chuo Kikuu cha St Paul cha Limuru. Maoni yaliyoonyeshwa hapa ni yake mwenyewe.